(1) Mamlaka ya utungaji wa sheria ya Jamhuri hii inatokana na wananchi na katika
kiwango cha kitaifa, yamekabidhiwa kwa na kutekelezwa na Bunge.
(2) Bunge hufuatilia uanuwai wa taifa, huwakilisha nia ya wananchi, na hutekeleza
Mamlaka yao.
(3) Bunge linaweza kukubali na kupitisha marekebisho kwenye Katiba hii na
kubadilisha mipaka ya kaunti kama inavyoagizwa katika Katiba hii;
(4) Bunge litalinda Katiba hii na kudumisha utawala wa kidemokrasia katika Jamhuri
hii.
(5) Hakuna mtu yeyote au asasi yoyote, isipokuwa Bunge, itakayokuwa na mamlaka ya
kuunda masharti yatakayokuwa na nguvu za kisheria nchini Kenya isipokuwa kwa
amri ya Katiba hii iliyokabidhiwa Bunge au kwa Sheria ya Bunge.
(6) Sheria ya Bunge, au sheria ya kaunti, inayoipatia asasi yoyote ya Serikali, afisa wa
Serikali, au mtu yeyote mamlaka ya kutunga masharti au sheria na kuipatia nguvu
za kisheria nchini Kenya, kama inavyokusudiwa katika Ibara ya (5), itaeleza bayana
na kwa hakika shabaha na malengo ya kukabidhiwa mamlaka haya, viwango vya
mamlaka, hali na upeo wa sheria zitakavyotungwa, na kanuni na viwango vya ubora
vinavyotumika kisheria na vilivyobuniwa chini ya mamlaka haya.
Soma kifungu kamili →